UTETEZI WA SHERIA ZA KIISLAMU
Muhtasari nne juu ya Sheria mbali mbali binafsi Za kiislamu
Kimeandikwa na: Allamah Sayyid Saeed Akhtar Rizvi
Kimetafsiriwa na: Dr. Mohamed S. Kanju
DIBAJI
Tunamshukuru Allãh (s.w.t.) na kwa baraka za Mtukufu Mtume (s.a.w.w.) na Ahlul~Bayt (a.s.) kwa kutujaalia kuweza kufanikisha juhudi zetu hizi katika kuchapisha kitabu hiki juu ya sheria za ki-Islamu.
Kitabu hiki kilochopo mikononi mwako ni tafsiri ya kitabu cha kiingereza kiitwacho In Defense of Islamic Laws kilicho andikwa na Allamah Al-Haj Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, Muasisi na Mhubiri Mkuu wa Mission hii.Kitabu hiki kimekua maarufu katika ulimwengu wa ki-Islamu.Watu wengi kutoka Afrika ya Mashriki wametuomba kukitafasiri katika lugha ya kiswahili.
Tunamshukuru Dr, Mohammad Salehe Kanju kwa kukitafsiri kitabu hiki katika lugha ya kiswahili.
Kwa manufaa ya wasomaji wetu tumeongeza makala juu ya Mahakama ya Kadhi ambayo ilitayarishwa na Mwandishi baada ya kitabu cha asili ya kiingereza kuchapishwa.
Mission inatoa shukurani zake za dhati kwa Bwana Mahmood Khimji ambaye kwa juhudi zake kitabu hiki kinawafikia wasomaji wetu mikononi na Sayyid Murtaza Rizvi kukipanga vizuri katika kompyuta na wale wote wanaotuunga mkono kwa njia moja au nyingine kwa kufanikisha kuchapishwa kitabu hiki, Tunamuomba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) awalipe malipo mema hapo Duniani na baadaye huko, Akhera.
HISTORIA FUPI YA MTUNZI WA KITABU HIKI
ALLAMAH SAYYID SAEED AKHTAR RIZVI
Hujjatul Islam Wal Muslimin Allamah Al-Haj Sayyid Saeed Akhtari Rizvi, alizaliwa katika Familia ya Maulamaa mwezi Mosi Rajab 1345 A.H. (5th Januari 1927 M.) katika mji wa Ushri Khurd, Wilaya ya Siwan, Bihar, India. Mazazi wake Marehemu Ustadul Ulamaa Sayedul Hukama Maulana Al-Haj Sayyid Abdul Hassan Rizvi (radhi za Mwenyezi Mungu Zimshukie) alikuwa Mmoja wa Maulamaa wakubwa wa India.
Allamah Rizvi alianza masomo yake katika mji wa Gopalpur makazi ya jadi yake na kuendelea huko Patna na Banaras. Alifaulu Shahada ya juu katika mtihani wa lugha za Kiarabu, Kiajemi na Kiurdu kutoka (Chuo Kikuu cha) Allahabad Board, U.P., na akafanikiwa kupata Shahada ya juu zaidi ya elimu ya dini - "Fakhru 'L-Afadhil" kutoka chuo cha Jami'ul 'Uloom Jawadia, Banaras.
Kuanzia ujana wake, alikuwa akijishughulisha kikamilifu katika jamii, elimu na kuinua dini ya Jumuiya. Katika mwaka wa 1948, alichukuwa nafasi ya baba yake kama Imamu wa Jumuiya huko Hallaur katika wilaya ya Basti, U.P. na akaendelea na nafasi hiyo hadi mwaka wa 1951. Kuanzia 1952 - 1959 alifanya kazi kama Mwalimu wa Urdu na Kiajemi katika shule ya Sekondari ya juu ya Husainganj (huko) Husainganj, Siwani.
Muda wa miaka yote hii alitumia likizo zake na wakati wake katika shughuli za Jumuiya kama kuendeleza shughuli za Anjumani Wazifa-e-Sadat-wa Momineen na Anjuma-e-Tarraqi-e-Urdu.
Katika Mwezi Desemba 1959, alikwenda Tanzania (wakati huo ikijulikana kama Tanganyika) ambako alihudumia kama Imam wa Jumuiya huko Lindi (1959-1962) Arusha (1963-1964) na Dar es Salaam (1965-1969).
Baada ya juma moja tu kuwasili kwake Afrika, alianza kujifunza lugha ya Kiswahili na kuangalia hali ya nchi kwa mtazamo wa kubalighisha Uislamu wa kweli miongoni mwa jamii ya wazawa (wa asili). Katika nyakati hizo kulikuwa hakuna Shia-Ithna-asheri hata mmoja mwenye asili ya Kiafrika katika bara lote. Katika mwaka wa 1962 alitayarisha mpango kwa ajili ya tablighi na akaupeleka kwa sekritariati ya Halmashauri Kuu ya Khoja Shia Ithnaasheri wakati huo ikiwa Arusha. Katika mwaka wa 1963 mpango huu ulijadiliwa kwa urefu. Katika hatua hiyo haukuweza kutekelezwa kama ilivyoshauriwa, lakini mwelekezo wa taratibu uliwekwa katika utekelezaji. Katika mwaka 1964 Sekritariati ilitayarisha taarifa (memorandum) iliyotegemea juu ya msingi wa taratibu yake ambayo iliwekwa katika agenda ya mkutano wa tatu wa mwisho wa mwaka wa muungano wa Jamati za Khoja Shia Ithna-asheri za Afrika (Federation of Khoja Shia Ithna-Asheri Jamaats of Africa) uliofanyika Tanga. Hivyo Bilal Muslim Mission ilizaliwa.
Kuanzia siku hiyo, Allamah Rizvi alitumia muda wake katika shughuli za Tabligh. Katika mwaka 1963 Bilal Muslim Mission of Tanzania ilisajiliwa. Wakati kazi ilipoongezeka, Marehemu Ayatullah Al-Uzma Sayyid Muhsin Al-Hakeem (Najaf, Iraq) aliamuru Halmashauri Kuu ya Khoja Shia Ithna-asheri ya Afrika kumtoa katika majukumu ya Jamaat, na kuanzia hapo gharama zote za Allamah Sayyid Rizvi zilichukuliwa na marehemu Ayatullah Al-Uzma Sayyid Muhsin Al-Hakeem na baada yake zikachukuliwa na marehemu Ayatullah Al-Uzma Sayyid Abul Qasim Al-Khu'i.
Kwa juhudi zake katika Mission hii makumi ya maelfu ya Waafrika wamekubali imani ya Shia pole pole kupitia mafundisho, maandishi na masomo kwa njia ya Posta, sasa Jumuiya ya Shia imestawi nchini Guyana chini ya Bwana Lateef Ali ambaye amefanikiwa kueneza ujumbe mpaka Trinidad na Tobago.
Mission ina kituo kwa ajili ya kufundishia Mubalighina mjini Dar es Salaam ambacho vile vile kina Bweni lenye nafasi. Kuna shule za chekechea, Msingi, Secondary na Madrasah ya Qur’ãn na Misikiti. Kwa nyongeza, Mission inaendesha masomo aina nne kwa njia ya Posta ambayo kwayo mwanga wa Ushia umefika mbali kwa marefu na mapana. Mission imechapisha vitabu zaidi ya miamoja na ishirini kwa Kiingereza na Kiswahili, sehemu kubwa ikiwa ni ya vitabu vya Allamah Rizvi au tarjuma yao.
Kuna Bilal Muslim Mission nchini Kenya (imeanzishwa sawia na Misheni ya Tanzania) Burundi, Malagasy na Msumbiji. Yakitiwa moyo na Bilal Muslim Mission of Tanzania, Mashirika yenye majina kama haya yameanzishwa nchini Seneghal,Naijeria,Ghana,Sweden na Marikani.
Katika mwaka wa 1978 alirudi na kukaa nchini India ambako alianza kuandika tarjuma ya Kiingereza ya Tafsir al-Mizan cha Marehemu Allamah Sayyid Muhammad Husayn at-Tabataba'i. Juzuu kumi za tarjuma hii zimekwisha chapishwa na World Organization For Islamic Service (WOFIS) Tehran Iran.
Mwezi Desemba 1980, alikwenda London kwa mualiko wa (Shirika la) Imam Sahebuz Zaman Trust. Kule London alikua pamoja na marehemu Hujjatul Islam Al-Mujahid Sayyid Mhadi al-Hakeem katika kuanzisha World Ahlul-Bayt (A.S.) Islamic League (WABIL) ni mmoja wa wadhamini watatu wa Shirika hili. Alikuwa Mkurugenzi wa Kamati ya maandalizi ambayo ilirasimu katiba ya WABIL na ilipanga mkutano wake wa kwanza wa katiba. Mkutano huu ulifanyika mwezi Augosti 1983 ambao kwayo wajumbe 80 kutoka nchi 30 walishiriki. Katika mkutano huo alichaguliwa kuwa mkurugenzi mkuu (wa shirika hilo).
Alirudi Tanzania mwaka 1986 kuendeleza shughuli za Bilal Muslim Mission of Tanzania na sasa hugawanya wakati wake kati ya Tanzania, India, na Canada.
Mwaka wa 1991 Ilianzishawa Ahlul~Bayt (A.S.) World Assembly (ABWA) Tehran,Iran na Allamah Rizvi alichguliwa mmoja wa wana kamati ya Halmashuri kuu na mjuube. Na vile vile ni Muasis na Mwenye Kiti wa Ahlul~Bayt (A.S.) Assembly of Tanzania.
Mwaka wa 1993 ameanzisha Bilal Charitable trust of India,Gopalpur. Hadi sasa zaidi ya Misikiti 25 na Hussaeinia zimejengwa na zaidi ya nyumba 30 za kuishi kwa watu ambao hawana makazi na vile vile shule za chekechea, Msingi, Secondary na teknolojia zimeanzishwa na Tasisi hii.
Allamah Rizvi ameanzisha Madrasa nyingi za Kidini na kufungua Markazi za Tablighi katika sehemu mbalimbali ulimwenguni, kati ya sehemu hizo ni India, Marekani, Uingereza, Canada, na nchi za Kiafrika.
Kufikia sasa ameandika vitabu 124 (78 kwa Kiingereza, 29 kwa Kiurdu, 11 kwa Kiarabu na 6 kwa Kiswahili) ambavyo 91 vimekwisha chapishwa na 6 vinachapishwa.Kwa muda huu, anajishughulisha katika kuandika vitabu 3 vya Kiingereza, Kiarabu na Kiurdu. Baadhi ya vitabu vyake vimetafsiriwa kwa lugha za Ki-Japan Ki-Indonesia, Ki-Thai, Ki-Burma, Ki-Urdu, Ki-Hindi, Ki-Gurjati, Ki-Sindhi, Ki-Ajemi, Ki-Swahili, Ki-Hausa, Ki-Shona, Ki-Taliani, Ki-Faransa Ki-Swidish Ki-Bosni Ki-Arabi Ki-Holanzi.
Vile vile amefanya kazi na baadhi ya Maulama wa Qum kuweka vizuri na kusahihisha Adh-Dhariah fi Tasanif As-shia, Kitabu kikubwa cha habari za vitabu na watungaji wake kilichoandikwa na marehemu Ayatullah Agha Buzrg at-Tehrani.
Amepewa Ijazat (Mamlaka) na Ma-Ayatullah wakongwe kumi na Tisa wa Najaf (Iraq) na Qum (Iran) kwa simulizi ya hadithi (riwayah) kwa mambo ya hukumu kwa Shariah na vile vile kushughulikia suala lolote ambalo kwalo ruhusa ya Mujtahid ni muhimu.
Ni mtaalam wa lugha. Huandika, huzungumza na kutoa mihadhara kwa Ki-Urdu, Ki-Arabu, Ki-Ingereza, Ki-Swahili na Ki-Ajemi. Vile vile anayo elimu (ya maandishi) ya Ki-Hindi na Ki-Gujarati. Mbali na ukubwa na upana (wa eneo) anaoshughulikia, na ziara za mara kwa mara ndani ya Afrika Mashariki, amezuru kama nchi 45 za Asia, Afrika, Ulaya na Marekani.
ORODHA YA BAADHI ZA VITABU VYA ALLAMAH RIZVI Kwa Kiingereza
1.Islam
2.Need of Religion
3. God : An Islamic Perspective
4.Justice of God
5. Prophethood
6. Imamate
7. Qur’an and Hadith
8. Day of Judgement
9. What a Muslim Should Know Believe
10. The Return of Al-Mahd
11. Elements of Islamic Studies
12. Fast
- Family Life of Islam
- Charter of Rights
- Hijab
- Muhammad (S.A.W.) is the Last Prophet
- The Holy Prophet
- Four California Lectures
- Taqiya
- Inner Voice
- Rulings On Morden Problems
- Islamic Laws
- In Defence of Islamic Laws
- Wahhabis’ Fitna Exposed
- On To The Right Path
- Pork
- Slavery
- Sects of Islam
- Shi’ite Sects
30. Your Questions Answered 1
31. Your Questions Answered 2
32. Your Questions Answered 3
33. Your Questions Answered 4
34. Your Questions Answered 5
35. Your Questions Answered 6
36. Your Questions Answered 7
- Your Questions Answered 8
- A Few Questions Answered
39. Fadak
40. The Ideal Islamic Government
41. Meaning & Origin of Shiism
42. The Quran Its Protection from Alteration
43. Prophecies About the Holy Prophet of Islam in Hindu Christian & Jewish Scriptures
- Some East African Ithna-Asheri Jamaats
- The Khoja Shia Ithna-Asheri Community in East Africa
- A Correspondence Between a Christian and a Muslim
- Selected Articals Vol 1
- Selected Articals Vol 2
UTANGULIZI
بسم الله الرحمن الرحيم
الحمد لله رب العالمين و الصلوة و السلام علی خير خلقه محمد و آله الطاهرين
Katika mwaka wa 1964, Bunge la Tanganyika lilipitisha Sheria ya “ki-Islamu” (Taarifa mpya) ambayo ilimpa uwezo Waziri anayehusika na mambo ya Sheria kutengeneza na kutangaza Taarifa ya Sheria ya ki-Islamu baada ya kushauriana na Wasomi wa sheria katika madhehebu za ki-Islamu. Kwa mujibu wa Gazeti la Standard Tanzania (13/ 7/67) liliandika : “Inafahamika kwamba Tanganyika ni nchi ya kwanza kupata kutekeleza zoezi la kupanga kanuni ya sheria ya ki-Islamu katika mfumo wa sheria iliamriwa halali. Taarifa hizi zitasaidia sana Mahakama ambazo hutegemea juu ya vitabu vya kiada”.
Khoja shia Ithna-asheri territorial council of Tanzania (Jumuiya ya Khoja shia Ithana-sheri) walilichukulia uzito suala hili. Bwana Mohamed G. Dhirani, aliyekuwa wakati huo Rais wa Baraza ya Jumuiya iliyotajwa, alinichukuwa mpaka kwenye Ofisi za Mwanasheria Mkuu, ambako nilimkuta wakili mkuu wa mradi huo. Alikuwa ni mwislamu wa Zanzibar. Alinishauri niandike kwa Kiingereza, sheria zote za Shi’a zihusikanazo na masuala haya kwa matumizi ya Ofisi yake. Hivyo niiandika “sheria za ki-Islamu zinazohusika na ndoa, kuvunjika kwa ndoa, makubaliano ya ndoa, wosia, mirathi na waqf”. Bwana Fida Hussein Abdallah Hameer, aliyekuwa Katibu wa Baraza wakati huo alitayarisha Sekretariati kwa ajili ya kusaidia.
Miwishowe makaratasi (yenye taarifa) yalimfikia Bwana Bashir Rahim, aliyekuwa mrasimu wa Bunge Muandamizi ambaye alikamilisha sura nne za ndoa (kama inavyokubalika na madhehebu makubwa matatu ya Sheria ya Uislamu - Shafii,Hanafi na Shi’a). Ilichapishwa chini ya mamlaka ya bwana Rashid Kawawa, aliyekuwa wakati huo makamu wa rais wa Tanzania, ambaye alikuwa anapasika vile vile na Idara ya Sheria. Ilitokea kama sheria ndogo zilizotungwa chini ya Taarifa rasmi mpya ya Sheria ya ki-Islamu (Na. 56 ya 1964) (Katika) Nyongeza ya Gazeti (La Serikali Na. 34 la 27 Juni 1967). Ilieleweka zile sura zilizobakia zinazohusu utunzaji wa watoto na talaka nk. zitachapishwa mwishoni mwa mwaka, na kisha hapo Sheria zitaanza kutekelezwa.
KUELEKEA KENYA
Sasa mandhari inahamia Kenya. Serikali ya Kenya wakati huo iliunda Tume juu ya sheria za ndoa, talaka na mirathi, chini ya uwenyekiti wa Mheshimiwa Jaji Spry wa Mahakama Kuu ya Kenya. Tume ilitakiwa itoe mapendekezo kwa ajili ya sheria mpya yenye uwezo mkubwa na kwa kadiri itakavyoweza kutumika kama sheria inayofanana ya ndoa, na talaka itumikayo kwa watu wote nchini Kenya. Ambayo itakuwa badala ya Sheria iliyopo juu ya suala lihusianalo na Sheria ya mila, Sheria ya “ki-Islamu”, (haswa ya kwetu) Sheria ya Baniani na Sheria za Bunge zinazohusika na kutayarisha rasimu ya Shria mpya; ikitoa kipaumbele mahususi kwa hadhi ya wanawake kuhusiana na ndoa na talaka katika jamii huru ya kidemokrasia.
Nilikwenda Mombasa Julai 1967 kwa mintaarafu fulani mingine na wahusika wa Supreme Council (Halmashauri Kuu ya Shia Ithna-asheri) walinichukuwa nikaonane na wakili ambaye alikuwa bingwa katika sheria binafsi za Uislamu. Kwa kuelezewa matukio ya Tanzania, aliniomba nimplekee nakala ya Sheria za “Ki-Islamu” ambayo nimeiandika kwa ajili ya Tanzania. Nami niliahidi hivyo.
Kabla ya hii, niliandika majibu kwa maswali ya Tume ambayo yalipelekwa kabla kwenye Tume.
Kurudi Dar es Salaam, nilikusanya taarifa ya Sheria za “Ki-Islamu” zilizotajwa (karibu karatasi ndefu mia moja, kurasa zilizopigwa mashine kwa karibu karibu) zikiwa zimerudufiwa, na kutumwa Halmashauri Kuu ya Khoja Shia Ithna-asheri.
Katika juma la tatu la Augusti 1967, niliitwa haraka Mombasa ambako tume ilikuwa ikae kwa ajili ya kusikiliza kuanzia 21/8/1967. Niliandika muhtasari (au taarifa) kwa ajili ya kuwasilisha mbele ya tume, ambayo ilikamilishwa baada ya majadiliano na maofisa wakuu watendaji (wa Halmashauri Kuu).
Muhtasari ule uliwasilishwa kwenye tume na kisha ukachapishwa katika “The Light” ya Julai – Augusti 1967. (Marehemu) Haji Mohamedali Meghji, Rais wa Halmashauri Kuu ya Khoja Shia Ithna-asheri aliandika barua iliyoambatanishwa ya maelezo (ya ziada) dondoo ambayo imechapishwa marudufu kabla ya muhtasari wa kwanza.
Mheshimiwa Jaji Spry alisikika akiwaambia wenzake baadae kwamba “watu hawa walijua kuhusu walichokuwa wakiongea”.
Muhtasari mwingine juu ya Sheria ya Mirathi ambao ulioandikwa na mimi, ulitumwa kwenye tume na kuchapishwa katika “The Light” ya Januari – Aprili 1968. Ni Muhtasari wa pili katika mkusanyo huu.
KURUDI TANZANIA:
Wakati matukio hayo hapo juu yalipokuwa yanafanyika nichini Kenya, ghafla Serikali ya Tanzania ilisimamisha zoezi la upangaji wa Kanuni (wa Sheria ya “ki-Islamu”).
Tume ya Kenya iliwasilisha taarifa yake na mapendekezo wakati Fulani katika mwaka wa 1969. Tarehe 10/9/69 Serikali ya Tanzania ilichapisha waraka (White Paper) No. 1 wa 1969 uliosema kwamba inataka kutunga Sheria ya Ndoa iliyo sawasawa (kwa wote), na ikatoa maelezo ya masharti iliyoyataka yawekwe kwenye Sheria iliyokusudiwa.
Pamoja na kuchapishwa kwa waraka, Serikali ilikaribisha maoni na mapendekezo kutoka kwenye Jumuiya na watu binafsi. Wakristo, Mabaniani na Maismailiya walichapisha maoni yao katika magazeti. Niliwafuata Bakwata kwa madhumuni haya; walikataa kwa mkato kabisa kuingilia mpango wa Serikali. Nilikuwa sina njia nyingine bali kuandika kwa niaba ya Shi’a Ithna-sheri tu. Maoni yalikuwa ya ukweli na pengine kifungu cha mwisho kilikuwa kikali kidogo. Nilipeleka mswada kwa Bwana Anverali M. Rajpar, aliyekuwa wakati huo Rais wa Khoja Shia Ithna-sheri Territorial Council of Tanzania, aliniambia niendelee na niuchapishe kwenye Gazeti la Standard kwa niaba ya Tanzania Council. Ilitokea katika Standard (Dar es Salaam) tarehe 8 Desemba 1969 (Jumatatu) na baadaye dondoo zake zilichapishwa katika “The Light” ya Desemba 1969. (Mswada) huu hutokea kama muhtasari wa tatu katika kijitabu hiki.
Wakati wa miezi ya baadaye, Halmashauri Kuu (Supreme Council) ilinitumia taarifa mbili za tume ya Kenya, nilishagazwa kuona kwamba karibu mapendekezo mengi ya waraka wa Tanzania yaliondolewa kutoka kwenye mapendekezo ya Tume ya Kenya.
Wakati naandika muswada wa Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971, katika mwanga wa waraka wa Serikali na maoni niliyopokea, Bwana Bashir Rahim, aliyekuwa wakati huo msawidi mkuu wa Bunge, alijaribu kwa uwezo wake kuingiza masharti ya Sheria za “ki-Islamu”. Kabla ya kukamilisha muswada huo, ulionyehswa kwa wanachuoni wa kila dini na madhehebu, na mabadiliko fulani yalifanywa kwa kutegemea juu ya ushauri wao.
HALI ILIYOPO SASA:
Serikali ya Tanzania sasa inataka kutunga Sheria ya Mirathi iliyo sawa kwa wote; ambayo itawapa wanawake kigawanyo sawa na kile cha wanaume. Wakati wanachuo wa “ki-islamu” (sio Bakwata) walipotoa kauli zao dhidi ya sheria hiyo, aliyekuwa wakati huo Rais (wa Jamhuri ya Tanzania) Mheshimiwa Al – Haji Ali Hasani Mwinyi aliwahakikishia kwamba rai haikuwa kubadilisha sheria ya “ki-Islamu”, bali kuweka haki ya mirathi kwa wanawake wale ambao hawana haki kama hizo kabisa – bali wao wenyewe wanachukuliwa kama bidhaa za mirathi.
Wakati huo huo katika mwaka wa 1990, mashirika mabalimbali ya “ki-Islamu” (Mbali na Bakwata) yalianza kufanya kampeni kwa ajili ya washichana wa “ki-Islamu” kuruhusiwa kuvaa Hijab mashuleni. Wawakilishi wao walikutana mara nyingi, na kutegemea juu ya majadiliano yao, niliandika Muhtasari juu ya Hijab na mirathi, ambao hatimaye uliwasilishwa kwa Rais Al-Haj Ali Hassan Mwinyi. (Muhtasari huo) umewekwa katika kijitabu hiki kama Muhtasari wa nne. Inafurahisha kuona kwamba Rais alitamka katika hotuba ya hadhara tarehe 10/8/1995 kwamba wasichana wa “ki-Islamu” sasa wanaruhusiwa kuvaa Hijab mashuleni; na Kaimu Kamishina wa Elimu alitoa mwongozo kwenye suala hili kwa taasisi za Elimu, ambao barua yake halisi yaweza kuonekana katika ukurasa ufuatao, na tarjuma yake ya kiingereza imetolewa mwiso wa kitabu hiki.
Bilal Muslim Mission of Tanzania inaona kwamba muhtasari hizi zina hoja zilizo wazi kuthibitisha kwamba Sheira za “ki-Islamu” zilizoanzia kutokana na hekima ya Mungu haziwezi kubadilishwa, na kwamba Sheria ya “ki-Islamu” ni mfumo pekee ambao huweza kutoa haki na uhuru katika jamii.
Ni kwa sababu hii kwamba Misheni hii imeamua kuchapisha Muhtasari nne pamoja katika kijitabu hiki. Nawashukuru kwa ari hii, na kuomba kwa Allah Subhanahu wa Ta’ala kuwapa tawfiq zaidi, na akifanye kitabu hiki kuwa njia ya mwongozo kwa Waislamu na kwa wasio Waislamu hali kadhalika.
و ما توفيقی الا با لله عليه توکلت و اليه انيب
Dar es Salaam Sayyid Saeed Akhtar Rizvi 31stOctober 1998
(1)
MUHTASARI JUU YA SHERIA ZA NDOA*
Dondoo kutoka barua iliyoambatanishwa : Muhtasari ufuatao uliandikwa na Maulana Sayyid Saeed Akhtar Rizvi kwa ajili ya kuwasilisha mbele ya tume juu ya Sheria za Ndoa, talaka na Mirathi, iliyowekwa na Serikali ya Kenya chini ya uweneyekiti wa Mheshimiwa Jaji Spry wa Mahakama Kuu ya Kenya.
Masharti ya Rejea kwa ajili ya Tume ni:-
“Kufikiria Sheria iliyopo ihusikananyo na Ndoa, Talaka na mambo yahusianayo na hayo;” “Kutoa mapendekezo kwa ajili ya Sheria mpya itoayo uwanja mpana na, kwa kadiri itakavyoweza kutekelezwa sheria ya Ndoa sawa kwa watu wote, na talaka itumikayo kwa watu wote nchini Kenya, ambayo itachukuwa nafasi ya sheria iliyopo juu ya suala lihusianalo na Sheria ya mila, Sheria ya ki-Islamu, Sheria ya ki-baniani na amri zinazohusika za Bunge na kutayarisha muswada wa Sheria mpya.”
“kutoa kipaumbele mahususi kwa hadhi za wanawake kaitka kuhusiana na ndoa na talaka katika jamii huru ya kidemokrasia”.
Tume ilituma maswali mapema kwa pande zote zinazohusika, na Halmashauri Kuu (Supreme Council) ikapeleka majibu yao (yalioandikwa na Maulana Sayyid Saeed Akhtar Rizvi) kwenye Tume kabla.
Tume ilikaa kwa ajili ya kusikiliza mjini Mombasa kuanzia tarehe 21 Augasti 1967. Ujumbe wetu ulitokea mbele ya tume tarehe 22 Augasti. Pamoja na Muhtasari, taarifa iliyobeba mambo mengi ya shria za ki-Islamu na mkusanyo wa hotuba juu ya Usul-Din “Islam” zote zikiwa zimeandikwa na kukusanywa na Maulana Sayyid Saeed Akhtar Rizvi, ziliwasilishwa mbele ya Tume.
Ni wazi kwamba juhudi ya Maulana katika suala hili imestahiki kusifiwa mno, na sisiti kukiri kwamba uwasilishaji ufuatao usingelifanikiwa bila muongozo na msaada wake.
Wajumbe wa msafara walikuwa, Maulana Sayyid Saeed Akhtar Rizvi,Mulla Asgherali M. M. Jaffer (Hon. Gen.Secretary – Mh. Katibu Mkuu),Bw. Hassan A. M. Jaffer (Mh. Mhazina Mkuu) Maulana Sheikh Maqbool Hussain (Mombasa) Bw. Bashir H. Pira na mimi mwenyewe.
Mh. Katibu Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Khoja Shia Ithna-asheri Mulla Asgheri M. M. Jaffer aliwasilisha kama msomaji wa Shia Ithna-asheri, na alisoma wasilisho mbele ya Tume.Vile vile alijibu maswali yaliyoulizwa na Tume, na kufafanua nukta mbali mbali zinazohusika na Ndoa, Talaka n.k. kwa mujibu wa madhehebu ya Shia.
MOHAMEDALI MEGHJI:
Rais, Shia Ithna-ashri-Halmashauri Kuu (ya Khoja) P. O. Box 1085, Mombasa.
*****
1.Kwa niaba ya Jumuiya ya shia Ithna-asheri ya Kenya, tunachukuwa fursa hii ya kufanya uwasilishaji huu kwa ajili ya kufikiriwa na Tume.
2.Katika uwasilishaji huu, tunakomea maelezo yetu kwenye Sheria za dini zilizofungana na Ndoa, Talaka, wosia na mirathi ya Madhehebu ya ki-Islamu ya Shia Ithna-asheri.
3.Inafahamika kwamba matatizo ya kijamii aina mbalimbali yatokeayo kwa kutmia vibaya au tafsiri potofu za mila, desturi au sheria za dini katika utekelezaji wa jumla, hutoa sababu kwa uwajibikaji wa makini kwa Serikali, na Serikali katika hamu yake kuwapatia watu wake ustawi katika suala hilo inakabiliwa na jukumu ngumu la Serikali la kutokomeza maovu ya kijamii. Juhudi yoyote katika muelekeo huu yafaa kuungwa mkono na hustahiki ushirikiano wote. Lakini tunahisi kwamba wazo la kutunga Sheria ya wote kuchukua mahali pa Sheria ya ki-Islamu iliyopo sasa sio sahihi.
Hata desturi za kimila (zisizo na mamlaka ya kidini) ni ngumu kubadilisha. Hii huwa hatari mno zaidi katika suala kama la Sheria ya ki-Islamu ambayo ni sehemu muhimu ya dini yetu, ambayo haikomei kwenye ibada tu. Sheria hizi haziwezi kuvunjwa bila ya kupata hisia ya hatia na dhambi.
Kwa hiyo, tunahisi kwamba njia nzuri “itakuwa kuacha mamia ya maua kuchanua.” Umoja wa Kitaifa hauhitaji kwamba raia wote yawapasa kuwa na lahaja inayofanana au imani ya dini inayofanana. Hivyo kwa nini inafikiriwa kwamba ni muhimu kuwa na Sheria ya Ndoa inayofanana na talaka ya kutumika kwa watu wote wa Kenya.
4.Sheria zetu za Shia Ithna-asheri hazikutegemezwa juu ya “Rai” (maoni) au “Qiyas” (anolojia). Zimetegemea kabisa juu ya Qur’an Tukufu na Hadith za Mtukufu Mtume na Maimamu wetu Kumi na Mbili.
Kwa vile tume inahusika na mambo ya Ndoa na Mirathi, lazima tuonyeshe kwamba kanuni za msingi na mambo mengi namna kwa namna ya mirathi yanaelezwa katika Qur’an Tukufu. Kusema kweli, maudhui hii imeshughulikiwa zaidi kwa ukamilifu katika Kitabu Kitukufu. Hali kadhalika, kanuni za msingi za ndoa na talaka zimetegemezwa juu ya Qur’an Tukufu.
Mambo ambayo hayako wazi katika Qur’an Tukufu yanaelezwa katika Hadithi kama ilivyotajwa hapo juu.
Wanachuoni wetu ambao wanaitwa MUJTAHID hawatoi hukumu yoyote kwa maoni yao, analojia (Qiyas) au (kwa) ijimai. Hakuna mamlaka kama hayo yaliyotolewa kwa yeyote katika Sheria ya madhehebu yetu. Wanaweza kutofautiana katika kutafsiri Hadith fulani zinazohusu baadhi ya mambo madogo, lakini hata hivyo tofauti hiyo ni tofauti katika tafsir, sio ya maoni.
Madhehebu ya Shia Ithna-ashri hufuata katika mambo yote ya dini hukumu za Mujtahid mkubwa wa zama. Anachukuliwa kuwa yeye ni mwakilishi wa Imamu wetu wa Kumi na Mbili na ni mtu wa mwisho juu ya mambo yote ya dini. Kwake yeye amekabidhiwa katika masuala fulani, mamlaka za ulezi wa watoto, ulinzi katika ndoa na talaka, utekelezaji wa Wosia na mali ya marehemu na mambo kama hayo.
5.Sheria ya ki-Islamu ya madhehebu ya Shia Ithna-asheri ni chombokilichofumwa vizuri. Hatuwezi kubadilisha au kurekebisha, moja au mbili ya mambo yake bila kuharibu ufumaji wote.
Kwa Mfano:-
[1] Hukumu za Ndoa na Talaka zinabeba uzito wa moja kwa moja juu ya uhalali au vinginevyo wa mtoto; juu ya wema au dhambi ya pamoja ya mwanaume na mwanamke; katika haki ya wao wenyewe kwa wenyewe ya mirathi na ile ya mtoto; mbali na kutokana na jamii na shida za kisheria.
[2] Katika sheria za ki-Islamu mtu hawezi kutumia kitu chochote kilichopatikana kiharamu (kwa maana ya kidini) amma kwa kilimwengu au kwa madhumuni ya kidini. Kwa hiyo, kama mabadiliko yanafanywa katika sheria za mirathi na mtu fulani anapewa zaidi kuliko mgao wake kwa mujibu wa Qur’an Tukufu, maisha yake yote yatakuwa duni. Maisha yake ya kila siku yatakuwa ni orodha ndefu ya kuchupa mipaka, Sala zake, Hija, chakula na mavazi vitakuwa haramu katika maana ya kidini.
Hivyo ni wazi kwamba mfumo wa Sheria ya ndoa, talaka na mirathi hauwezi kubadilishwa; vinginevyo hii itaanzisha muingilio wa moja kwa moja katika dini yetu.
6.Kuhusu hamu ya Tume “Kutoa kipaumbele kwa hadhi ya wanawake katika kuhusiana na Ndoa na Talaka katika jamii huru ya kidemokrasia”.
Tunataka kuwakilisha kama ifuatavyo:- (a) katika sheira ya madhehebu yetu mwanamke anazo haki hizo upendeleo na ulinzi wa salama tangia Karne ya Kumi na nne, nyingi ya hizo hazikufikiriwa katika Jamii zisizo za ki-Islamu mpaka Karne iliyopita na baadhi ya hizo ziko mbele ya inayoitwa zama ya kisasa.
(b) Uislamu kwa mujibu wa madhehebu ya Shia, umempa mwanamke haki ya kufanya mkataba yeye mwenyewe katika Ndoa kama ni mtu mzima na makanifu.
- Uislamu umempa mwanamke kitambulisho cha
kujitegemea. Mwanamke wa ki-Islamu anamiliki mali yake mwenyewe hata baada ya kuolewa, na mume hawezi kuingilia.
(d) Mwanamke anaweza kumfungulia mume wake mashtaka, anawezakutoa ushahidi dhidi yake. Anarithi kutoka kwa mume kwa haki na mwanaume kutoka kwa mwanamke.
Haki hii, ya wote pamoja ya mirathi (kurithiana) ilitolewa wakati hakuna jamii kamwe ilifikiria kuhusu haki hii.
7.Mgao wa mwanamke kwa kawaida ni, nusu ya ule (mgao) wa mwanaume. Lakini hii ni mantiki kabisa. Uislamu umemfanya mwanaume kuwa na jukumu la kutunza familia. Hakuna mzigo kama huo uliowekwa juu ya mwanamke. Hata mke tajiri anahusika kupata matunzo yake kutoka kwa mume wake ingawa anaweza kuwa ni maskini. Kwa vile matunzo ya familia ni jukumu la mwanaume, amepewa mgao marudufu karibu katika mirathi yote.
Vile vile, mwanamke hupata mahari ambayo hutoka kwa mume kwenda kwa mke. Kwa hiyo uwiyano wa mgao uliowekwa katika Qur’an Tukufu ni wa haki zaidi.
8.Sheria ya Uislamu ihusianayo na Wosia haimruhusu mtu kuusia zaidi ya thuluthi moja ya mali yake kamili. Hivyo hali ya kifedha ya wale watakao kuwa warithi siku zote inalindwa na mbali ya kutwaliwa kokote isivyo haki na yeyote. Usalama huu bado unakosekana katika jamii nyingi ambazo huruhusu mtu kutoa mali yote kwa mgeni haswa.
9.Sasa tunakuja kwenye baadhi ya mambo ya Ndoa:-
(a)MITALA : Jamii ya Waafrika ilikuwa, na kwa kiwango fulanini jamii ya kimitala. Uislamu vilevile huruhusu mitala. Umeruhusu wake wanne kwa wakati mmoja na imeamuru usawa katika kuwahudumia wake wote.
(b)Yapasa ikumbukwe kwamba mitala sio kitu cha lazima wala sio kitu kinachotetewa. Ni ruhusa tu pamoja na ukomo Fulani na masharti. Na katika baadhi ya mazingira ruhusa hii imethibitisha manufaa mazuri mno.
Kwa mfano, kama mke ana ugonjwa sugu au ni mgumba au kwa sababu nyingine fulani haiwezekani kwa wawili hao kuishi kama mume na mke. Suluhisho litolewalo na jamii fulani ni kumtaliki mke na kuoa mwingine. Lakini je, hii ni haki? Je, ni wema au uadilifu kumfukuza mwanamke katika hali ya uzee au katika umri wake wakati kutoka kwenye nyumba yake, kwa sababu ame kuwa mgonjwa siku zote au ametokea kuwa mgumba? Uislamu hupinga ukatili huo kwa kuruhusu mitala.
10.(a) TALAKA: Hakuna haja kusisitiza kwamba katika hali fulani talaka ndio suluhisho pekee lililobakia kwa wawili hao (mume na mke). Manufaa ya mfumo wa talaka yanaweza kuonekana kutokana na ukweli kwamba hata Baniani na Wakristo wengi wamelazimika kwa nguvu ya moja kwa moja isio epukika kutnga sheria za talaka.
(b) Ni lazima tuonyeshe kwenye wakati wa mwanzo kwamba madhehebu ya Shia-Ithanaseri ya ki-Islamu imeweka kanuani ngumu zilizotegemea juu ya Qura’n Tukufu na Hadithi, kuhusiana na talaka.
(c) Talaka imetangazwa na Mtukufu Mtume kuwa ni kitu kilichotwezwa katika halali zote.
(d) Qur’an Tukufu imeweka mfumo wa usuluhisho wakati wowote kukiwa kuna kutokuelewana kati ya mume na mke.
(e) MASHARTI YA TALAKA: Talaka inaruhusiwa mradi tu inatamkwa mbele ya watu wawili mashahidi. “Adil” (watu wamuelekeo thabiti) ambao husikiliza maeneno na kuelewa asili au chanzo cha talaka. Talaka lazima itamkwe katika utaratibu uliothibitishwa,
Zaidi ni lazima vile vile kwamba mume awe mtu mzima, mwenye akili timamu na mwenye kuelewa vizuri atendaye kwa utashi wa uhuru wake mwenyewe, na sio katika mshituko wa hasira au kutishwa. Nakwamba lazima awe na nia ya dhahiri ya kuvunja ndoa.
Kwa kadiri mwanamke anavyohusika,yeye wakati wa Talaka lazima awe katika hali ya tohara na kwamba talaka haiwezi kutamkwa hata wakati wa tohara ambao kwamba mume amekutana naye kimwili.
Kama moja ya masharti yaliyotajwa hapo juu yakivunjwa Talaka itakuwa batili na kutenguka.
(f) Talaka tatu haziwezi kutolewa kwa wakati mmoja. Kama mtu atasema kwamba anatoa talaka tatu, hata moja haitakuwa halali.
(g) Katika hali nyingi, talaka inaweza kutenguliwa, na mume ana lazimika kumtunza mke aliyetalikiwa wakati wa kipindi cha “Iddat” (kwa kawaida ni miezi mitatu) katika nyumba yake; vinginevyo ahiari kutoka (mwenyewe).
(h) Wakati wa kipindi kilichotajwa cha “IDDAT” mume anayo haki ya kutengua talaka kwa maneno au kitendo na kutakuwa hakuna haja ya taratibu zozote.
Kanuni hizi ngumu zimekuwa siku zote zikitekelezwa na madhehebu yetu. Shukurani kwa Shariat yetu, talaka katika madhehebu ya Shia-Ithanasheri ziko mara chache sana.
11.HAKI YA MWANAMKE KUHUSIANA NA UVUNJANI WA NDOA: Mwanamke hakupewa haki ya kumpa talaka mume wake. Sababu yeneyewe sio ngumu sana kuelewa. Familia ni msingi wa jamii ya binadamu na kwa vile kila jamii huhitaji mamlaka ya mwisho kuiweka katika mpango ulioandaliwa vizuri. Familia lazima vile vile ipate kiongozi mkuu. Sheria ya ki-Islamu imetoa nafasi hiyo kwa mume, na mume amepewa haki ya kutoa talaka.
Lakini mke ana haki ya kudai talaka katika hali nyingi: Km: (1) Anaweza akaomba Khula ambayo inaweza kukubalika juu yake na mume; (2) Anaweza kumuomba Mujtahidi kumpa talaka katika hali ambako mume ametoweka, au akapuuza kumtunza.
(3) Katika hali ya mume yakuwa mwenda wazimu, imma imetokea kabla au baada ya ndoa, ana haki ya kuifuta ndoa bila haja yoyote ya kupeleka kesi kwa Mujtahid.
(4) Na anaweza kuibatisha Ndoa baada ya kuipeleka kesi kwa Mujtahid, kama mume ni hanithi.
12.Katika uwasilishaji wetu, tulionyesha mapema kwamba sheria sawa kwa wote katika jamii ya kilimwengu kama hii ya Kenya haina umuhimu kwa umoja wa kitaifa. Sasa tunaomba kuwasilisha kwamba kuishi pamoja, kwa amani na urafiki miongoni mwa watu walioambatanishwa kwenye imani za dini mbalimbali na sheria kunaweza kupatikana tu kama uhuru utatolewa kwao kutekeleza sheria kama hizi, na kutenda kimujibu (kama itakikanavyo).
Haitakuwa nje ya sehemu (ya maudhui) kutaja hapa kwamba Uislamu una seti ya theolojia inayojumuisha mambo yote ya maisha. Na kwamba amri zake na maelekezo hayakomei kwenye ibada za sala za kila siku na maombi pekee. Ni mfumo wa maisha ambao hutoa huduma ya mipangilio namna namna kwa jaamii, ndoa, maadili, na hali kadhalika uendeshaji wa biashara katika maisha ya kibinadamu.
Pengine itakuwa ni kitu cha kuvutia kwamba hivi karibuni Tanzania imechapisha “Taarifa ya sheria ya ki-Islamu. “ Huu ni utungaji mdogo wa Sheria chini ya “Taarifa mpya ya shria ya ki-Islamu” (No. 56 ya 1964). Nyongeza ya Gazeti (la Srikali) No. 34 ya 27 Juni, 1967 yahusika. Hatua hii iliyokuja wakati mzuri katika Tanzania imethibitisha kwamba nchi yoyote inayopigania uhuru wa kuabudu na utekelezaji wa dini inaweza kwa usalama kuweka sheria mbali mbali kuhusiana na Ndoa, Talaka, Mirathi au mambo yoyote kama hayo. Vile vile huonyesha kwamba hatua kama hiyo inatekelezeka. Tunaweza kuongeza kwamba vile vile hudokeza kwamba mpangilio kama huo unasaidia kwenye kuelewa vizuri na uhusiano katika nchi ambako mazingira ya maridhia yanatakiwa yafanyike, na tunaweka mikononi mwa tume kupendekeza hatua kama hiyo nchini Kenya.
13.Kujaribu kuweka mpaka kati ya Qur’an Tukufu na Sheria ya ki-Islamu kamwe hakuwezi kufikirika. Jaribio lolote la kuvuruga au katika maneno ya masharti ya rejea ya Tume, “Kubadilisha Sheria ya ki-Islamu” kutakuwa hakukubaliki. Kama ilivyoelezwa hapo juu, sheria ya ki-Islamu imetegemezwa juu ya Qur’an Tukufu na kubadilisha Sheria ya Kiislamu ni sawa sawa na kubadilisha Qur’an Tukufu.
14.Tumewasilisha maswali yaliyotumwa na Tume yakiwa yamekamilishwa ipasavyo sambamba pamoja na mpangilio wa sheria ya ki-Islamu (katika Kiingereza) kwa mujibu wa Sheria ya Madhehebu ya Shia kuhusiana na Ndoa, uvunjaji wa Ndoa, Wosia, Mirathi, Makubaliano na Wakf; na tutafurahi kujibu maswali yoyote yajitokezayo kutoka humo na kuwasilisha ufafanuzi utakiwao.
MOMBASA, 22 AGOSTI 1967.