Na heri yoyote muitendayo - kuwatendea mayatima na wananwake – basi Mwenyezi Mungu anaijua. Kwa ufupi maana ya Aya ni kuwa waislamu walimtaka Mtume kuwabainishiahukumu ya wanawake. Mwenyezi Mungu (s.w.t) akamwambia Mtume wake:
waambie Mwenyezi Mungu amewabainishia sehemu ya hukumu hii na sasa anawabainishia sehemu nyingine, la muhimu kwenu ni kufanya uadilifu na kuitumia hukumu hiyo. Kisha akawabainishia Mwenyezi Mungu (s.w.t.), katika Aya inayofuatia hukumu ya mwanamke, anayehofia unashiza wa mumewe na kuachana na mumewe.
وَإِنِ امْرَأَةٌ خَافَتْ مِن بَعْلِهَا نُشُوزًا أَوْ إِعْرَاضًا فَلاَ جُنَاْحَ عَلَيْهِمَا أَن يُصْلِحَا بَيْنَهُمَا صُلْحًا وَالصُّلْحُ خَيْرٌ وَأُحْضِرَتِ الأَنفُسُ الشُّحَّ وَإِن تُحْسِنُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا {128}
128.Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza, basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu; Na suluhu ni bora. Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo. Na mkifanya wema na mkajihifadhi, basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa myatendayo.
وَلَن تَسْتَطِيعُواْ أَن تَعْدِلُواْ بَيْنَ النِّسَاء وَلَوْ حَرَصْتُمْ فَلاَ تَمِيلُواْ كُلَّ الْمَيْلِ فَتَذَرُوهَا كَالْمُعَلَّقَةِ وَإِن تُصْلِحُواْ وَتَتَّقُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ غَفُورًا رَّحِيمًا {129}
129.Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake hata mkikamia. Basi msipondokee kabisa kabisa, mkamwacha (mwingine) kama aliyetundikwa. Na mkisikilizana na mkamcha Mungu, basi Mwenyezi Mungu ni mwingi wa maghufira mwenye kurehemu
وَإِن يَتَفَرَّقَا يُغْنِ اللّهُ كُلاًّ مِّن سَعَتِهِ وَكَانَ اللّهُ وَاسِعًا حَكِيمًا {130}
130.Na watakapotengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa Mwenye hekima.
UNASHIZA WA MUME
Aya 128 - 130
MAANA
Ikiwa mke atahofia mumewe kuwa nashiza au kumtelekeza.
Unashiza unaweza kuwa kwa mke kwa kumnyima unyumba mumewe au kutoka nyumbani bila ya idhini ya mume.Yametangulia maelezo ya unashiza wa mke katika kufasiri Aya ya 34 ya Sura hii.
Pia unashiza unaweza kuwa kwa mume kwa kumuudhi mke na kuacha kumpa matumizi au kumnyima siku akiwa na mke zaidi ya mmoja. Aya hii inaelezea hofu ya mke kwa unashiza wa mumewe au kumtelekeza. Makusudio ya kutelekeza ni kumwepuka kwake kunakoonyesha kumchukia. Ama kwenda kwenye shughuli zake na matatizo yake, lazima mke amvumilie na kumstahmilia madamu hamchukii.
Basi hapana vibaya juu yao kusikilizana kwa suluhu.
Ikiwa mke anahofia kuwa unashiza wa mumewe utasababisha talaka au kuwa katika hali ya kufungika - si kuwa na mume wala kuachwa, basi hapana ubaya kwa mume wala kwa mke kuafikiana wenyewe au kupitia kwa mtu. Waafikiane na kusikilizana, kuwa mume aache kumnyima haki zake, ili abakie katika hifadhi yake na waishi maisha ya utulivu.
Na suluhu ni bora kuliko kutengana na talaka. Kuna Hadith isemayo: "Halali inayochukiza zaidi kwa Mwenyezi Mungu ni talaka." Ni vizuri tueleze kuwa anachokitoa mke kwa ajili ya talaka si halali ila kwa kuridhia nafsi yake. Mwenyezi Mungu anasema: "… Kama wakiwatunukia kitu katika hayo mahari, basi kuleni kwa raha na kunufaika." (4:4)
Na nafsi zimewekewa mbele uchoyo.
Yaani uchoyo daima uko mbele katika nafsi haumwepuki hata wakati wa kutoa, ile hali ya jakamoyo anayoihisi mtoaji na kuificha wakati wa kutoa ndio uchoyo wenyewe na makusudio ya kauli yake Mwenyezi Mungu "na nafsi zimewekewa mbele uchoyo." Mke haiachi haki yake kwa urahisi wala mwanamume hasamehi badali. Tusisahau kuwa Aya tukufu imezungumzia matatizo ya unyumba. Ama ikiwa unyumba hauna matatizo hakuna lolote la kuwajibisha kutoa kitu bali hakuna kati ya mume na mke anayeona kuwa kitu ni chake.
Na mkifanya wema na mkajihifadhi basi Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa muyatendayo.
Huu ni mwito kutoka kwa Mwenyezi Mungu (s.w.t.) kwa mume na mke kufanya kila juhudi amfanyie wema mwenzake na ajichunge na sababu za kukosana na kutengana.
Wala hamtaweza kufanya uadilifu baina ya wanawake hata mkikamia.
Kufanya uadilifu baina ya wake kuko aina mbili: Kuna kule kunakowezekana, kama kufanya usawa katika matumizi na mazungumzo mazuri. Na kuna ambako kuko nje ya uwezo wa binadamu, kama vile mapenzi ndani ya moyo na hata kujamii pia. Mume anaweza kusisimuliwa na mke, kiasi ambacho yule mwingine hamsisimui vile.
Uadilifu baina ya wanawake unaotakiwa ni katika matumizi ambao uko chini ya uwezo. Ama uadilifu katika mapenzi na mfano wake, mtu hakalifishwi nao. Na hii ndiyo inayotofautisha baina ya Aya hii na ile Aya ya tatu katika Sura hii isemayo: "Na kama mkihofia kutofanya uadilifu, basi ni mmoja …"
Imam Jafar as-Sadiq anasema: "Ama kauli yake Mwenyezi Mungu: ‘Mkihofia kutofanya uadilifu’ anakusudia kutoa matumizi; na ama kauli yake; 'Hamtaweza' anakusudia mapenzi.” Na sisi ni katika wale wanaoamini kabisa kuwa hakuna kitu kigumu kukipata kuliko uadilifu. Kwa hakika yake hasa na kiini chake ni kujikomboa na matamanio; kama ilivyoelezwa katika baadhi ya Hadith kwamba mwadilifu ni yule mwenye kuhalifu mapenzi yake na akamtii Mola wake. Wala hawi na haya ila aliyejitakasa.
Basi msipondokee kabisa kabisa.
Kwa mke mnayempenda na mwingine mkamnyima haki zake.
Mkamwacha (mwingine) kama aliyetundikwa akawa si mke aliyeolewa anayepata haki zake, wala si mtalikiwa anayeweza kuolewa na mwingine anayemtaka.
Na watakapotengana, Mwenyezi Mungu atamtosheleza kila mmoja kwawasaa wake.
Inatakikana kabla ya chochote mume na mke wajaribu kuondoa tofauti zao na mambo yanayosababisha kutengana. Kwa sababu suluhu ni bora. Ikiwa haiwezekani, basi talaka ni bora kuondoa madhara zaidi; na fadhila ya Mwenyezi Mungu na riziki yake itawaenea wote, wawe pamoja au watengane. Mwenyezi Mungu anaweza kumpa mtalikiwa mume bora kuliko wa kwanza; na anaweza kumpa mtaliki mke bora kuliko wa kwanza.
Kwa ufupi ni kwamba yote yaliyotangulia yanazunguuka kwenye mzunguuko mmoja tu ambao ni "kushikana kwa wema na kuachana kwa wema." Kushikana ni bora ikiwa hakuna ufisadi na kuachana ni bora ikiwa kuna ufisadi; kama ambavyo Mwenyezi Mungu ameumba dawa ya kuponesha magonjwa ya mwili, vile vile ameweka dawa ya maradhi ya kijamii.
وَللّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَلَقَدْ وَصَّيْنَا الَّذِينَ أُوتُواْ الْكِتَابَ مِن قَبْلِكُمْ وَإِيَّاكُمْ أَنِ اتَّقُواْ اللّهَ وَإِن تَكْفُرُواْ فَإِنَّ لِلّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَكَانَ اللّهُ غَنِيًّا حَمِيدًا {131}
131.Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini. Na hakika tuliwaamrisha waliopewa Kitabu kabla yenu na nyinyi kwamba, mcheni Mwenyezi Mungu. Na kama mkikufuru, basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na ardhini. Na Mwenyezi Mungu ni mkwasi mwenye kusifiwa.
وَلِلّهِ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَكَفَى بِاللّهِ وَكِيلاً {132}
132.Na ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyo ardhini, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa mlinzi.
إِن يَشَأْ يُذْهِبْكُمْ أَيُّهَا النَّاسُ وَيَأْتِ بِآخَرِينَ وَكَانَ اللّهُ عَلَى ذَلِكَ قَدِيرًا {133
133.Akitaka atawaondolea mbali, enyi watu alete wengine. Na Mwenyezi Mungu ni muweza wa hilo.
مَّن كَانَ يُرِيدُ ثَوَابَ الدُّنْيَا فَعِندَ اللّهِ ثَوَابُ الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ وَكَانَ اللّهُ سَمِيعًا بَصِيرًا {134}
134.Anayetaka malipo ya duniani, basi yako kwa Mwenyezi Mungu malipo ya duniani na akhera na Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia mwenye kuona.
NI VYA MWENYEZI MUNGU VILIVYOMO MBINGUNI NA VILIVYOMO ARDHINI
Aya 131 - 134
MAANA
Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.
Katika juzuu ya kwanza na juzuu hii, tumezungumzia kuhusu kukaririka katika Qur'an. Sasa tutazungumzia kukaririka kwenye Aya hasa hii , kwa sababu ni Aya iliyotajwa na kurudiwa zaidi katika Qur'an . Kisha tutadokeza kukaririka kwa namna maalum ambayo imetajwa kwa kunakiliwa mara mbili katika Aya moja na kurudiwa mara ya tatu katika Aya inayoifuatia moja kwa moja bila ya kuweko kati kitu kingine.
Ama sababu za kukaririka kwake kwa ujumla ni kwamba maudhui yake ni ulimwengu ambao pamoja na vilivyomo ndani yake unatolea dalili kuwapo Mwenyezi Mungu na sifa zake; kama elimu, uweza, matakwa na hekima. Ni dalili inayokusanya aina za dalili zote na vyenye kutolewa dalili. Kwa hiyo kukumbuka Aya hii ni kukumbuka kuwapo Mwenyezi Mungu na utukufu wake.
Ama kutajwa kwake hapa mara tatu, ni ishara ya faida tatu: Kwanza: Mwenyezi Mungu katika Aya iliyotangulia amesema: "…Atamtosheleza kila mmoja kwa wasaa wake" Kwa hiyo dalili hii imenasibiana na wasaa huu kuwa ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini.
Pili: Amesema: Kama mkikufuru basi ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini.
Yaani yeye hamhitaji mwenye kukufuru kwa sababu vilivyomo mbinguni na ardhini ni vyake.
Tatu: Amesema Mwenyezi Mungu: Ni vya Mwenyezi Mungu vilivyomo mbinguni na vilivyomo ardhini, na Mwenyezi Mungu atosha kuwa mlinzi. Akitaka atawaondelea mbali, enyi watu na alete wengine.
Makusudio ni kwamba Yeye ni muweza wa kuwamaliza waasi na kuwaleta watiifu; kwa sababu ni vyake vilivyomo mbinguni na ardhini. Kwa hiyo kila moja katika mara hizo tatu ina sababu yake na kukutanishwa na faida mpya.
Anayetaka malipo ya duniani, basi yako kwa Mwenyezi Mungu malipo ya duniani na akhera.
Yaani malipo ya duniani na akhera yanawezekana kupatikana pamoja na imani na takua. Mwenye kudhani kuwa malipo ya duniani hayawi pamoja na takua, basi huyo amekosea. Kwa sababu hakuna kitu chochote kinachotengeneza vizuri maisha ya hapa duniani ila kitakuwa kinakubaliwa na dini bali kinaamrishwa na kuhimizwa na hiyo dini, lakini kwa sharti moja tu; kuwa kufanikiwa kwake kusiwe ni uovu kwa mwingine na utukufu wake usiwe ni utwevu wa mwingine.
Kwa hivyo malipo ya duniani na akhera hayagongani; isipokuwa kugongana kunatokea baina ya dhulma na malipo ya akhera - baina ya ghushi, hadaa na unyang'anyi na vilevile radhi za Mwenyezi Mungu, neema zake na pepo yake.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاء لِلّهِ وَلَوْ عَلَى أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالأَقْرَبِينَ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقَيرًا فَاللّهُ أَوْلَى بِهِمَا فَلاَ تَتَّبِعُواْ الْهَوَى أَن تَعْدِلُواْ وَإِن تَلْوُواْ أَوْ تُعْرِضُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا {135}
135.Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa wa karibu. Akiwa ni tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi. Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu. Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo.
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ آمِنُواْ بِاللّهِ وَرَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِي نَزَّلَ عَلَى رَسُولِهِ وَالْكِتَابِ الَّذِيَ أَنزَلَ مِن قَبْلُ وَمَن يَكْفُرْ بِاللّهِ وَمَلاَئِكَتِهِ وَكُتُبِهِ وَرُسُلِهِ وَالْيَوْمِ الآخِرِ فَقَدْ ضَلَّ ضَلاَلاً بَعِيدًا {136}
136.Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kabla. Na mwenye kumkakataa Mwenyezi Mungu na Malaika Wake na vitabu vyake na siku ya mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali.
KUWENI IMARA NA UADILIFU
Aya 135 - 136
BAINA YA DINI NA WATU WA DINI
Sijaona Aya katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu inayoambatana na dini ila ninahisi umbali na tofauti iliyopo baina ya dini kama alivyoipanga katika Kitabu chake na dini kama tunavyoitekeleza sisi. Sisi tunazungumzia dini na kuitolea mwito kuwa imetoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba sisi hatuna lolote katika amri yake na ni watumwa wa dini, kama tulivyo watumwa wa Mungu.
Hayo ndiyo tuyatangazayo na kuyaeleza. Lakini dini tunavyoitangaza na tabia zetu tunazodai ni za kidini ni wapi na wapi! Na ni kinyume waziwazi. Na hii haifahamishi chochote zaidi ya kuwa sisi, kwa hakika na hali halisi ilivyo, ni wanafiki.
Ni sawa tutambue hivyo au tusitambue. Lau kama tutaifasiri dini kuwa Mwenyezi Mungu amelipa uwezo baraza la dini litunge sharia za halali na haramu, kama wanavyodai baadhi ya watu wa dini, basi hapo ingelikuwa dini inakwenda sambamba na tabia zetu. Ama tukisema kuwa dini ni ya Mwenyezi Mungu na inatoka kwa Mwenyezi Mungu, kisha tusiende sambamba na hayo katika tabia na vitendo vyetu, basi huo ni unafiki hasa.
Enyi mlioamini! Kuweni imara na uadilifu mtoao ushahidi kwa ajili ya Mwenyezi Mungu ijapokuwa ni juu ya nafsi zenu au wazazi wawili na jamaa wa karibu.
Katika Aya nyingine Mwenyezi Mungu anasema: " Na msemapo semeni kwa uadilifu hata kama ni jamaa wa karibu, Na tekelezeni ahadi ya Mwenyezi Mungu …" (6: 152)
Maana yake ni kuwa dini inatuhukumu sisi, baba zetu na watoto wetu; na kwamba ikitokea mgongano baina ya masilahi ya kiutu na dini, basi ni juu yetu kutanguliza ya dini; hata kama hili litapelekea kufa; kama alivyofanya Bwana wa mashahidi Husein bin Ali (a.s.) Lau mtu atalinganisha hakika hii ya Qur'an na tabia zetu ataona kuwa sisi tunaathirika na masilahi yetu na masilahi ya watu wetu, kuliko masilahi ya dini.
Na akiendelea kufanya utafiti zaidi ataamini kuwa kiini cha kwanza na cha mwisho cha dini kwetu ni masilahi na manufaa tu, si Kitabu cha Mwenyezi Mungu wala Sunna ya Mtume wa Mwenyezi Mungu.
Hivi ndivyo tulivyo au ndivyo walivyo wengi katika sisi, lakini hatutambui hili wala kulizindukia. Kwa sababu ubinafsi umetawala akili zetu na ukatenganisha hali halisi zetu na nafsi zetu na kutuziba macho tusione haki. Pia imetupa ndoto ya kuwa dini ya Mwenyezi Mungu ni masilahi yetu hasa, vinginevyo si chochote.
Nayasema haya si kwa kumwekea nongwa yeyote au kuwa na msukumo wowote. Kwani mimi, kwa fadhila za Mwenyezi Mungu, sina haja na yeyote katika viumbe vyake Mwenyezi Mungu. Lakini hivi ndivyo ninavyohisi na wanavyohisi wengine wachunga haki.
Mimi nionavyo ni kuwa hakuna budi kuweko na marekebisho ya hisia hii; kama ambavyo ninaitakidi kuwa hakuna dawa ya ugonjwa huu ila kujituhumu sisi wenyewe; na ninaitakidi kuwa sisi ni wa kawaida tu kama wengine tuna hawaa na mapondokeo ambayo ni lazima tujihadhari nayo na tuyahalifu. Ninasema haya nikijua kuwa ni kama kupiga kelele za kutaka msaada jangwani. Kwa sababu ni kilio kutoka kwa nafsi zetu kwenda kwa nafsi zetu, ambazo ndizo adui mkubwa katika maadui zetu.
Akiwa tajiri au fukara basi Mwenyezi Mungu anawastahiki zaidi.
Kila mtu katika wanadamu ana hali ya kukubali heri na shari wakati huo huo anaumbile la kuchagua heri kuliko shari, kiasi ambacho lau ataachwa na umbile lake, angelifanya lile analoitakidi kuwa ni heri; wala hawezi kuiepuka ila kwa sababu za nje ya dhati yake na maumbile yake.
Wanavyuoni wa elimu ya sifa za Mwenyezi Mungu wametolea dalili hakika hii kwamba mwenye akili lau atahiyarishwa baina ya kusema uongo apewe pesa, basi angelichagua ukweli kuliko uongo.
Kwa hiyo mwenye akili hasemi uongo ila kwa sababu; kama vile hofu, tamaa, kupendelea jamaa wa karibu, kuchukia adui, kuwahurumia mafukara au kujipendekeza kwa tajiri. Na amesema mkuu wa wasemaji; Akiwa – wenye kushuhudiwa - ni tajiri au fukara, basi Mwenyezi Mungu anawastahikizaidi. Yaani kwamba yeye ni mwenye kurehemu zaidi mafakiri kuliko sisi na ndiye anayejua maslahi yake na maslahi ya tajiri. Sisi wajibu wetu ni kusema haki tu ni sawa iwe itawasaidia au la.
Ingawaje Mwenyezi Mungu hakutaja sababu zinazosababisha kupotoka zaidi ya kustahiki tajiri au kumuhurumia fakiri, lakini sababu ni ya kiujumla. Haki inapaswa kufuatwa hata kwa maadui wa dini.
Basi msifuate hawaa ili mfanye uadilifu. Yaani, mtakuwa watu wa uadilifu kwa kuacha hawaa na kwenda kinyume nayo. Imesemekana kuwa tafsiri yake ni kukadiria kuchukia kwa maana ya msifuate hawaa mkaacha uadilifu. Yaani nyinyi mnafuata mapenzi kwa kuchukia uadilifu na kwamba Mwenyezi Mungu amewakataza hilo. Lakini tafsiri ya kwanza ndiyo iliyo karibu zaidi.
UADILIFU
Wamehitalifiana mafakihi katika maana ya uadilifu na wakarefusha maneno. Kuna katika wao mwenye kusema, ni dhahiri ya uislam bila ya kudhihirisha ufasiki, Mwingine akasema, ni tabia iliyomo ndani ya nafsi inayopelekea kufanya wajibu na kuacha haram, wa tatu akasema, ni sitara na kujistahi, wa nne akasema ni kuacha madhambi makubwa na kutoendelea na madogo. Katika kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: "Msifuate hawaa ili mfanye uadilifu."
Ni kuonyesha kuwa uadilifu ni kuhalifu hawaa. Amirul-muminin Ali (a.s.) alimsifu ndugu yake, kwa Mwenyezi Mungu, katika aliyomsifu kuwa; "Alikuwa akijiwa ghafla na mambo mawili huangalia lipi lililo karibu zaidi na hawaa kisha akalikhalifu."
Na akasema: "Mwanzo wa uadilifu wake ulikuwa ni kukanusha hawaa ya nafsi yake."
Amesema Mjukuu wake, Imam Jafar as-Sadiq: "Ama katika mafaqih atakayekuwa anaichunga nafsi yake, mwenye kuihifadhi dini yake, mwenye kukhalifu hawaa yake, mwenye kutii amri ya Mola wake basi ni juu ya watu kumfuata."
Na mkiupotoa au mkaachana nao basi Mwenyezi Mungu ana habari ya myatendayo. Yaani msicheleweshe au kuacha kutoa ushahidi. Kisha akatoatisho na kiaga kwamba mwenye kuyafanya hayo Mwenyezi Mungu anamjuana atamwadhibu.
Enyi mlioamini! Mwaminini Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake na Kitabu alichokiteremsha kabla.
Mtu anaweza kuamini Muumbaji na kukanusha utume na vitabu vya Mwenyezi Mungu. Na anaweza akakubali utume wa baadhi na baadhi ya vitabu; au kukanusha kuwapo Malaika au Siku ya Mwisho. Aya hii imebainisha nguzo za imani ambazo ni wajibu kuzikubali kila mwenye kuacha shirki na ulahidi na kuziamini zote sio baadhi ya sehemu zake. Nguzo zenyewe ni kumwamini Mwenyezi Mungu na mitume yake yote, vitabu vyake na Malaika wake na pia Siku ya Mwisho.
Kwa hiyo makusudio ya neno 'wale walioamini,' ni wale walioacha ushirikina na ulahidi. 'Na wale walioamini' la pili ni imani ya uhakika, sio kudumu imani na kuthibiti kwenye imani kama walivyosema wafasiri, Makusudio ya Mtume wake, ni Muhammad (s.a.w.). Na Kitabu ambacho amemteremshia Mtume wake ni Qur'an na Kitabu alichokiteremshia kabla, ni kila Kitabu cha Mwenyezi Mungu alichokiteremsha kabla ya utume wa Muhammad (s.a.w.)
Na mwenye kumkataa Mwenyezi Mungu na Malaika waake na vitabu vyake na Siku ya Mwisho, basi amepotea upotevu ulio mbali.
Aya hii ni dalili wazi kwamba kuamini ghaibu ni nguzo katika nguzo za Kiislamu na kwamba asiyeamini si Mwislamu. Umetangulia mfano wa Aya hii pamoja na tafsiri yake katika sura 2: 285.
إِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ ثُمَّ كَفَرُواْ ثُمَّ آمَنُواْ ثُمَّ كَفَرُواْ ثُمَّ ازْدَادُواْ كُفْرًا لَّمْ يَكُنِ اللّهُ لِيَغْفِرَ لَهُمْ وَلاَ لِيَهْدِيَهُمْ سَبِيلاً {137}
137.Hakika wale walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru, hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaghufiria wala kuwaongozea n j i a .
بَشِّرِ الْمُنَافِقِينَ بِأَنَّ لَهُمْ عَذَابًا أَلِيمًا {138}
138.Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.
الَّذِينَ يَتَّخِذُونَ الْكَافِرِينَ أَوْلِيَاء مِن دُونِ الْمُؤْمِنِينَ أَيَبْتَغُونَ عِندَهُمُ الْعِزَّةَ فَإِنَّ العِزَّةَ لِلّهِ جَمِيعًا {139}
139.Ambao huwafanya makafiri ndio marafiki badala ya waumini. Je wanataka kwao utukufu? Basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.
HAWATHIBITI KWENYE UKAFIRI WALA IMANI
Aya 137 - 139:
LUGHA
Asili ya neno Bishara ni habari njema za kufurahisha ambazo zinadhihirisha furaha katika ngozi bashar (bashar) ya uso. Mtu akimwambia mwenzake nakupa bishara basi anajua kuwa kuna jambo la kufurahisha. Halitumiwi neno hilo katika jambo la kuchukiza ila pamoja na kukutana na neno jingine, kama vile kauli yake Mwenyezi Mungu: Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.
MAANA
Hakika wale walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru, hakuwa Mwenyezi Mungu ni mwenye kuwaghufiria wala kuwaongozea njia.
Mtu anaweza kuamini dini yoyote miongoni mwa dini au itikadi yoyote katika itikadi. Hapo atashikilia na kujadiliana na watu wa dini nyingine au fikra nyingine kwa ajili ya dini yake. Kisha anasoma na kufanya utafiti ikambainikia makosa. Anaachana na fikra yake ya kwanza na kujiunga na watu wema ambao jana walikuwa ni katika maadui zake wakubwa.
Ni juu ya hawa kumkubali na kumpokea; wala hakuna haki yoyote ya kumwaibisha na kupinga mageuzi yake ya kufuata njia sahihi iliyomdhihirikia. Bali ni wajibu kumsifu na kumtukuza, kwa sababu mtu kuacha makosa ni utukufu na kuendelea nayo ni udhalilifu.
Hii ni ikiwa atathibiti na kudumu kwenye imani yake mpya. Ama akigeuka na kurudia sera yake ya kwanza, kisha akarudi tena, akarudia… Akafanya hivi mara nyingi. Huyu ni wajibu kumtoa na kumtupa. Bali ni wajibu kumwadhibu kwa adhabu kali. Hii ndiyo hali waliyokuwa nayo watu wa dini na wakuu wa madhehebu ya kisiasa tangu zamani na sasa. Kwa sababu kugeukageuka kwake huku kunafahamisha tu, kuwa yeye anafanya masihara na vitimbi na ni mzushi mwongo anayejiingiza katika ufisadi na upotevu na kuzidisha dhambi na upotevu kila anapoingia na kutoka.
Huyu na mfano wake ndio wanaokusudiwa na Mwenyezi Mungu Mtukufu anaposema: "…Walioamini kisha wakakufuru kisha wakaamini kisha wakakufuru kisha wakazidi kukufuru " Kwa sababu ya mchezo huu na kujigeuzagueza, Mwenyezi Mungu hakuwa ni mwenye kuwasamehe maadam wanayumbayumba na kugeukageuka baina ya ukafiri na imani; wala kuwaongozea njia kwa sababu wamepotea njia kwa kuchagua uovu baada ya kuijua njia na kuifuata. Kwa ufupi ni kwamba muumin ni yule anayethibiti kwenye imani yake hata hali ikigeuka vipi. Ama yule anayertadi mara kwa mara, basi yeye ana hali mbaya kuliko yule aliyethibiti katika ukafiri na ulahidi.
Wape bishara wanafiki kuwa wana adhabu iumizayo.
Razi anasema: "Mwenyezi Mungu ametumia neno 'bishara' kwa adhabu kwa istihzai sawa na msemo: 'salaam zako ni kipigo." Ilivyo, ni kwamba mfumo wa Qur'an uko mbali na stihzai. La karibu zaidi ni kwamba makusudio ya bishara ni habari tu na inawezekana kulitumia neno hilo katika jambo la kuchukiza kwa kuambatana na jambo lenyewe; kama tulivyotangulia kueleza katika kifungu cha lugha.
Ambao huwafanya Makafiri ndio marafiki badala ya waumini. Je, wanataka kwao utukufu, basi hakika utukufu wote ni wa Mwenyezi Mungu.
Kila mmoja katika sisi anataka atajike katika maisha haya. Baadhi ya watu wanaweza kupupia kutaka umashuhuri kwa kufanya wema au kwa elimu. Lakini wengine hutaka utukufu na umashuhuri kwa kitu chochote kitakachokuwa; wanauza dini yao kwa shetani kwa ajili ya kupata umashuhuri; humfanya shetani ndio rafiki wa kumsikiliza na kumtii.
Ndipo hapa likaja swali la kusuta na kukanusha kutoka kwa Mola mtukufu kuwa je, wanataka utukufu kutoka kwa shetani na marafiki zake wadhalilifu. Je, utukufu unaweza kupatikana bila ya imani na takua? Uislamu kwa utukufu wake umedhalilisha dini zote, vipi utukufu utatafutwa kwa mwenye kuukanusha?
Waumini waliokusudiwa na Mwenyezi Mungu katika kauli yake "badali ya waumini" ni wale ambao uislamu umetukuka kwa ajili yao. Kwa sababu wao wameutukuza na kuuweka juu kwa jihadi yao na kujitolea kwao mhanga.
Tumezungumzia kuhusu kuwafanya marafiki makafiri katika tafsir (3: 28)
وَقَدْ نَزَّلَ عَلَيْكُمْ فِي الْكِتَابِ أَنْ إِذَا سَمِعْتُمْ آيَاتِ اللّهِ يُكَفَرُ بِهَا وَيُسْتَهْزَأُ بِهَا فَلاَ تَقْعُدُواْ مَعَهُمْ حَتَّى يَخُوضُواْ فِي حَدِيثٍ غَيْرِهِ إِنَّكُمْ إِذًا مِّثْلُهُمْ إِنَّ اللّهَ جَامِعُ الْمُنَافِقِينَ وَالْكَافِرِينَ فِي جَهَنَّمَ جَمِيعًا {140}
140.Na amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki kwamba mtakaposikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na kuchezwa shere, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine. Hivyo hakika nyinyi mtakuwa mfano wao. Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote katika Jahannam.
الَّذِينَ يَتَرَبَّصُونَ بِكُمْ فَإِن كَانَ لَكُمْ فَتْحٌ مِّنَ اللّهِ قَالُواْ أَلَمْ نَكُن مَّعَكُمْ وَإِن كَانَ لِلْكَافِرِينَ نَصِيبٌ قَالُواْ أَلَمْ نَسْتَحْوِذْ عَلَيْكُمْ وَنَمْنَعْكُم مِّنَ الْمُؤْمِنِينَ فَاللّهُ يَحْكُمُ بَيْنَكُمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَلَن يَجْعَلَ اللّهُ لِلْكَافِرِينَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ سَبِيلاً {141}
141.Ambao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, huseme: Je hatukuwa pamoja nanyi. Na ikiwa Makafiri wamepata sehemu, husema: hatukuwa ni waweza wa kuwashinda tukawakinga na waumin? Mwenyezi Mungu atahukumu baina yenu siku ya kiyama na Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumini.
MSIKAE NAO MPAKA WAINGIE KATIKA UZUNGUMZI MWINGINE
Aya ya 140 - 141
MAANA
Na amekwisha wateremshia katika Kitabu hiki kwamba mtakaposikia Aya za Mwenyezi Mungu zinakanushwa na kuchezwa shere, basi msikae pamoja nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine.
Aya hii ilishuka Madina, inawakumbusha waislamu Aya iliyoshuka Makka isemayo: "Na unapowaona wale ambao wanaziingilia Aya zetu, basi jitenge nao mpaka waingie katika mazungumzo mengine; na kama shetani akikusahaulisha, basi usikae baada ya kukumbuka pamoja na watu wadhalimu." (6:68)
Ama sababu ya ukumbusho huu ni kuwa baadhi ya Waislamu - kama ilivyoelezwa Katika Tafsiri mbali mbali - walikuwa wakikaa katika vikao vya washirikina huko Makka waliokuwa wakiingilia kumtukana Muhammad (s.a.w.) na kuicheza shere Qur'an. Waislamu wakati huo walikuwa wanyonge hawawezi kuwakanya; ndipo ikashuka Aya hiyo (6: 68), kuwahadharisha waislamu waepukane na washirikina na kuwaamrisha wasikae nao wanaposikia kufru na kuchezwa shere Aya za Mwenyezi Mungu.
Siku zikapita na waislamu wakahamia Madina; huko nako kulikuwa na mayahudi na wanafiki, waliodhihirisha uislamu na kuficha ukafiri. Baadhi ya waislamu wakarudia mwenendo wao wa kwanza, wakakaa na mayahudi na wanafiki waliokuwa wakiutusi uislamu na Mtume wake; ndipo ikashuka Aya hii, ambayo tunaifasiri, ili kuwakumbusha waislamu Aya ile iliyoshuka Makka na kuwaamrisha kujitenga nao.
Sababu yoyote ya kushuka Aya itakavyokuwa au wanaoambiwa, itakuwa Aya ni ya ujumla inayofahamisha wajibu wa kujitenga na kila mwenye kuingia katika mazungumzo ya batili. Wajibu huu hauhusiki na ambaye alikuwa akikaa na makafiri Makka au na wanafiki Madina tu, ingawaje iko katika kuhusika si kwa ujumla. Hadith inasema: "Upweke ni bora kuliko rafiki mwovu." Nyingine inasema: "Tahadharini na kukaa na maiti." Akaulizwa ni akina nani hao maiti?
Akasema: ni kila mwenye imani potofu, dhalimu katika hukumu”. Katika Nahjul Balagha imeelezwa: "Kukaa na watu wapuuzi kunasahaulisha imani na kumkurubisha shetani."
Hivyo hakika nyinyi mtakuwa mfano wao
Mwenye kuridhia ukafiri ni kafiri, na mwenye kurdhia dhambi naye ana dhambi kwa namna yoyote atakayokuwa; kwa maafikiano ya mafakihi na Maulama. Imekuja Hadith Mutawatir isemayo: Mwenye kufanya dhulma, mwenye kumsaidia na mwenye kuiridhia ni washirika," hasa mwenye kuridhia ukafiri. Katika Nahjul-Balagha imeelezwa: "Mwenye kuridhia vitendo vya watu ni kama mwenye kuingia ndani yake na kila mwenye kuingia ana dhambi mbili: dhambi ya kutenda na dhambi ya kuridhia."
Hakika Mwenyezi Mungu atawakusanya wanafiki na makafiri wote katika Jahannam. Ambao wanawangojea mkipata ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu husema; Je, hatukuwa pamoja nanyi? Na ikiwa makafiri wamepata sehemu, husema: hatukuwa ni waweza wa kuwashinda tukawakinga na waumin.
Aya hii inachora picha ya hali ya wanafiki wakati wa vita vya waislamu na washirikina. Kwa ufupi picha yenyewe ni kwamba wanafiki walikuwa wakitoka pamoja na waislamu katika kwenda vitani ili wakaharibu na kuchafua safu za waislam. Wakati huo huo wanajionyesha kuwa wao wametoka kuwasaidia waislam; na kungoja, ikiwa ushindi ni, waislamu wakisema 'sisi tuko pamoja nanyi kwa hiyo sisi na nyinyi ni washirika katika ngawira.' Ikiwa ushindi ni wa washirikina husema, "sisi tulikuwa majasusi" Basi yako wapi malipo? Wanaishika fimbo kati kati.
Ufasaha zaidi niliousoma kuhusu wasifu wa wanafiki, ni ule aliousema Amirulmumiinin Ali (a.s.): "Wameiandalia kila haki batili, na kila msimamo upotofu, na kila mlango ufunguo, na kila usiku taa."
Hawa wapo kila siku na idadi yao inaongezeka katika miji ya kiarabu siku hadi siku, tangu ilipojitokeza dhahabu nyeusi (petrol). Wakafanya uzalendo kuwa ni nembo kama walivyojionyesha waislamu wakati wa Mtume. Wapigania ukombozi wakiwashinda wanyonyaji na walanguzi, wanafiki huwaambia: Je, hatukuwa pamoja nanyi? Na kama wanyonyaji wakifanikiwa huwaambia: Je, hatukuwazuia wapigania ukombozi wasiwafikie.
Unaweza kuuliza: Kwa nini Mwenyezi Mungu (s.w.t.) ametumia ushindi kwa waislamu na kupata sehemu kwa makafiri?
Jibu: Ushindi wa waislam ndio ushindi wa haki ambao unadumu na kubaki maadamu watu wake wanafuata desturi ya Mwenyezi Mungu na amri yake katika kujiandaa. Kwa hiyo ikanasibu kuleta ibara ya ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ama ushindi wa batili ni ushindi wa muda usiodumu, unaondoka mbele ya watu wa haki, kama wakiungana kwa Jihadi.
Walikwishasema zamani; "Dola ya batili ni saa moja na dola ya haki ni mpaka Kiyama."
Wala Mwenyezi Mungu hatawafanyia makafiri njia ya kuwashinda waumin.
Mafakihi wameitolea dalili Aya hii kwamba Mwenyezi Mungu (s.w.t.) hakuweka sharia inayofanya mamlaka au usimamizi wa asiyekuwa mwislamu kwa mwislamu; Na wameitolea hukumu nyingi; kama vile kuwa baba wa mtoto akiwa mwislamu na mama yake sio mwislamu, mama hana haki ya kumlea. Kwa sababu mtoto hufuata dini iliyo tukufu zaidi anayoifuata mmoja wa wazazi wawili na hukumu yake ni hukumu ya waislamu.
Hukumu nyingine ni kuwa haijuzu kwa mwislamu kuwausia watoto wake wasimamiwe na asiyekuwa mwislmau; na akifanya hivyo basi wasia umebatilika. Hukumu nyingine waliyoitoa katika Aya hiyo ni kuwa, baba anakuwa na usimamizi kwa watoto wake kama wana dini moja. Ama wakiwa ni waislamu na baba si mwislam hatakuwa na usimamizi juu yao. Nyingine ni kuwa hukumu ya hakimu asiyekuwa mwislamu haitekelezwi kwa haki ya mwislamu, hata kama ni haki na mengine mengi.
إِنَّ الْمُنَافِقِينَ يُخَادِعُونَ اللّهَ وَهُوَ خَادِعُهُمْ وَإِذَا قَامُواْ إِلَى الصَّلاَةِ قَامُواْ كُسَالَى يُرَآؤُونَ النَّاسَ وَلاَ يَذْكُرُونَ اللّهَ إِلاَّ قَلِيلاً {142}
142.Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye mwenye kuwahadaa. Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu. Wanajionyesha kwa watu Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu.
مُّذَبْذَبِينَ بَيْنَ ذَلِكَ لاَ إِلَى هَـؤُلاء وَلاَ إِلَى هَـؤُلاء وَمَن يُضْلِلِ اللّهُ فَلَن تَجِدَ لَهُ سَبِيلاً {143}
143.Ni vizabizabina baina ya huku na huko. Na ambaye Mwenyezi Mungu amemwacha kupotea huwezi kumpatia njia
WANAMHADAA MWENYEZI MUNGU NA ATAWALIPA KWA KUHADAA KWAO
Aya 142 - 143
MAANA
Hakika wanafiki wanamhadaa Mwenyezi Mungu, na hali yeye ndiye mwenye kuwahadaa.
Makusudio ya kuhadaa kwao ni kule kuonyesha imani kwa Mtume na kuficha ukafiri. Kwa sababu mwenye kumhini Mtume ndio amemhini Mwenyezi Mungu. Kama alivyosema Mwenyezi Mungu: "Hakika wale wanaokuunga mkono kwa hakika wamemuunga mkono Mwenyezi Mungu…" (48: 10)
Makusudio ya kuwa Mwenyezi Mungu anawahadaa ni kwamba yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu atawaadhibu kwa hadaa yao na unafiki wao.
Na wanapoinuka kwenda kuswali, huinuka kivivu.
Wataichangamkiaje na wao wanaikanusha? Hawatarajii thawabu kwa kuitenda wala adhabu kwa kuiacha; isipokuwa wanaitekeleza kwa kuwinda dunia tu na kuifanya ni nyenzo ya uchumi. Mwenyezi Mungu anasema: "Kwa hakika hiyo Swala ni ngumu isipokuwa kwa wanyenyekevu."(2: 45)
Unaweza kuuliza: Mtu akiswali kwa kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu na pamoja na hayo anapenda watu wamuone, ili wamhisabu katika watu wema au asituhumiwe kuwa aniipuuza dini. Je hii itakuwa ni ria?
Jibu: Hapana! Maadamu msukumo wa kwanza ni wa amri ya Mwenyezi Mungu na radhi zake; mengine yanafuatia tu, Imam as-Sadiq (a.s.) aliulizwa kuhusu mtu ambaye anafanya jambo la kheri, kisha akafurahi kwa kuonwa na mtu mwingine akilifanya jambo hili (nini hukumu ya mtu huyo)? Imam akajibu: "Hapana ubaya kwa hilo, ikiwa hakuifanya kwa hilo, kwani hakuna mtu asiyependa Mwenyezi Mungu amdhihirishie kheri mbele ya watu,."
Wanajionyesha kwa watu.
Kwa sababu wao huswali kwa ajili ya kuwinda na kupata faida.
Wala hawamtaji Mwenyezi Mungu ila kidogo tu. Yaani wakati wa kujionyesha kwa watu. Ama wakiwa peke yao, hawamtaji kabisa. Imam Jafar as-Sadiq (a.s.) anasema: "Mwenye kujionyesha (ria) ana alama tatu: Anakuwa mvivuakiwa peke yake, anachangamka akiwa na watu na hupenda kusifiwa kwa asilolifanya."
JE WATU WOTE HUJIONYESHA
Unaweza kuuliza: Hakuna yeyote anayedhihirisha ukweli wake kwa watu na kuwaambia kila analoitakidi. Ni nani anayeweza kumwambia kila mtu anayoyajua. Na akifanya hivyo, basi atahisabiwa katika wenda wazimu, bali ni nani ambaye - mara nyingine - hafanyi asiyoyapenda na kuyataka? Kisha utaziepuka vipi desturi na maadili ya jamii?
Je, unaweza kumwambia mtu uliyekutana naye, ambaye humpendi, akakwambia 'natamani kukuona,' na wewe umwambie: nachukia kukuona? Na kama utamwambia hivyo je unavyoona wewe au waonavyo watu utakuwa uko sawa? Mwisho je watu wote wanafanya ria (kujionyesha), kwa sababu hawaitakidi yote wayasemayo; wala hawaamini yote wayafanyao?
Jibu: Kuna tofauti baina ya Ria na Mudarat. Ria ni kudhihirisha unafiki na uzushi ili uwe pamoja na wema na wewe si katika wao. Na Mudarat ni kuwa mpole na kutowachukilia na kuamiliana na watu bila ya kulenga chochote zaidi ya kutaka kuishi nao katika uelewano na maafikiano.
Ni kweli kuwa mara nyingine unafanya mambo kufuata desturi ya jamii; ukapongeza, kutoa rambi rambi au kutabasamu na kumheshimu mtu kwa jamala tu si kwa kuamini, lakini jambo hili ni salama halina tashwishi yoyote.
Wala halihisabiwi kuwa ni ria maadam kulifanya kwako kunaafikiana na jamii. Vilevile si wajibu juu yako kama utatokewa na kosa - hakuna maasum – kulitangaza kwa watu. Ndio ni wajibu kuwadhihirishia usafi sio makosa. Vilevile ni kweli kuwa unasema uongo unapomwambia unayemchukia 'mimi nakupenda,' lakini ni uongo ulio katika masilahi na hulka njema. Mwenyezi
Mungu anasema: "Na semeni na watu kwa uzuri" (2: 83)
Je hukuona vipi Mwenyezi Mungu alivyopiga mfano wa neno zuri? Ni kama mti mzuri mizizi yake ni imara na matawi yake yako mbinguni." (14:24) "Nendeni kwa firaun hakika yeye amepetuka mpaka. Kamwambieni maneno laini huenda akaonyeka au akaogopa. " (20: 44 - 45)
Kuna Hadith isemayo: "Tamko jema ni sadaka, hupewa thawabu alisemaye, thawabu za wenye fadhila na ihsan." Hadith nyigine inasema: "Ameniamrisha Mola wangu kuwachukulia watu upole (Mudarat), kama alivyoniamrisha faradhi (wajib)."
Wamekongamana mafakihi kwamba uongo ni wajibu ikiwa utakuwa ni kutetea nafsi isiyo na hatia na kuiepusha na maangamivu. Na kwamba ukweli ni haram katika ufitini na usengenyaji. Kwa hiyo mfitini ni mkweli na msengenyaji ni mkweli, lakini wanashutumiwa mbele ya Mwenyezi Mungu na mbele za watu.
Baada ya yote hayo ni kwamba ria ya haramu ni ile ya kudhihirisha mambo asiyokuwa nayo mbele za watu; anajionyesha kuwa ana kheri ili apate hadhi ya watu wema na huku mwenyewe ni katika waovu wafisadi.
-Maandiko ya Qur'an na Hadith yako kwenye misingi ya kufanya lenye masilahi na kuacha lenye uharibifu. Penya masilahi ni amri na penye uharibifu ni katazo. Kwa hiyo ndio ikajuzu kusema uongo pamoja na masilahi na ikawa haramu kusema ukweli pamoja na uharibifu wenye masengenyo na upeke peke.